Familia moja katika kijiji cha Onyakoboke, Wadi ya Riana katika kaunti ya Kisii inahuzunika baada ya kupokea Habari iliyodai mwana wao ameaga dunia kule Al Hofuf, Saudi Arabia mwezi jana.

Kulingana na familia hiyo ya Mary Bonareri na Christopher Nyanchabera, walipokea simu mnamo Octoba 9 2020 ikiwajulisha binti yao, Janet Nyanchabera, amefariki kutokana na Covid-19 kwenye nchi hiyo ya Kiarabu ambako alikuwa ameajiriwa kama dereva.

Hata hivyo, siku 30 baadaye, familia ya Mary haijaamini ujumbe huo kwani hawajapokea maelezo kamili kutokana na madai ya kifo cha mwanao.

“Janet alielekea Saudi kutafuta kazi ili asaidie familia yetu ambayo ni maskini. Mwezi moja umepita tangu tupokee simu kwamba amekufa kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Tumekesha hapa nyumbani tukiomba na kutumaini kuwa msamaria mwema atajitokeza na kutuletea mwili wa mtoto wangu nyumbani. Lakini tunaendelea kupoteza matumaini kwa vile ni vigumu kuomboleza bila maiti. Hata tumeanza kufikiria kubomoa vibanda kwenye boma ndiposa tukae tukijua hatuna matanga,” alisema Bi Bonareri kwa uchungu mwingi


Mary Bonareri akiwa nyumbani kwake. Picha: Cindy Odinga

“Aliposafiri, hatukupata kuelewa ajenti yake alikuwa nani kwa vile aliondoka kisirisiri. Ninaomba serikali ya Kenya itusaidie,” Bi Bonareri liongeza.

Walipotembelewa na 47 reporters, Christopher Nyanchabera ambaye ni babake Janet, alikuwa na mshtuko mkubwa hivyo hangeweza kuzungumza .

Kulingana na Denise Nyanchabera, kakake mdogo Janet, yeye ndiye alikuwa wa mwisho kuwasiliana na dadake Septemba 23 2020. Siku hiyo, Janet alimfichulia kuwa alikuwa mgonjwa. Hata hivyo, Denise anasema dadake hakumweleza anaugua ugonjwa upi.

Janet hakuwahi wasiliana tena na mtu yeyote wa familia. Aliyepiga simu, akitumia nambari +966 53 00331777 , alikuwa mwajiri wake “boss” Janet, akieleza kifo cha mwendazake.

Bosi huyo hajakuwa tayari kusimulia ni vipi Janet aliaaga dunia.

Nduguye mkubwa Janet, Jared Oyugi, anakumbuka alikuwa amepinga kusafiri kwa dadake kuelekea Ughaibuni na hata kuficha cheti chake cha kuzaliwa. Hata hivyo, dadake hakusikiliza mawaidha yake. Jared anasema Janet alijitafutia vyeti feki na hata kubadilisha jina lake likawa Janet Wanjiku Nyamburi.

Licha ya hayo, Bw Oyugi anaiomba serikali ya Kenya, ikishirikiana na ile ya Saudi Arabia, ziwasaidie na maelezo tosha kuhusu kifo cha mwanao ili waweze kurejelea maisha yao ya kawaida.

“Ombi letu ni kwamba tumzike hapa nyumbani na tumuage kwa mara ya mwisho; ili tuweze kuridhika kwamba ametuacha. Tulijulishwa kwamba alikufa kutokana na Covid-19 ila ni vigumu kuamini kwa vile hakuna mtu yeyote katika familia yetu ambaye ameona hata picha ya maiti. Hatujaamini kwamba amekufa,” Bwana Oyugi aliambia¬† 47 reporters


Waliokongamana nyumbani kwa Mwendazake wasijue la kufanya. Picha: Cindy Odinga

Mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya mwendazake Joseph Mukora alisema jamii yao haijawahi kufkiwa na msiba kama huu wa mmoja wao kufariki akiwa nje ya nchi. Anaiomba serikali iingilie kati, iwapo ni kweli Janet ameshafariki.

“Matumaini yetu ni kumzika nyumbani kwa wazazi wake kulingana na mila na desturi za jamii ya Abagusii lakini hatuna uwezo wa kifedha,” Bw Mukora alisema.

Hadi sasa, mipangilio ya mazishi imesimama. Hawajui la kufanya.

By Henix Obuchunju

Multimedia journalist

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *